WHO yataka kulindwa kwa watumishi wa afya wanaofanya kazi kwenye mazingira hatarishi

18 Agosti 2014

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema kuwa wakati umefika kwa dunia kuachana na vitendo vya kuwadhuru watumishi wa afya wanaohudumu kwenye maeneo yanayokumbwa na migogoro ya vita .

WHO imesisitiza kuwa ni muhimu watumishi hao wakatoa huduma zao kwa uhuru hasa wakati huu ambapo dunia imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la mahitaji ya dharura. Taarifa kamili na George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Wakati dunia ikijiandaa kuadhimisha siku ya kimataifa ya misaada ya Usamaria mwema ambayo huadhimishwa kila mwaka Agosti 19, ripoti zinaonyesha kuwa watumishi wengi wa afya wamekuwa wakiandamwa na matukio ya  mashambulizi katika maeneo yanayokumbwa na migogoro.

Kwa maana hiyo WHO imesema kuwa itatumia siku hiyo kutuma ujumbe maalumu kwa dunia juu ya kuwajali watumishi wa afya ambao wengi wao wamekumbwa na matukio ya mashambulizi hasa huko Syria, Gaza, Jamhuri

ya Afrika ya Kati, Iraq na Sudan Kusini.

Kitisho kingine kinachowaandama watumishi hao wa afya ni kuhusiana na kuzuka kwa virusi vya Ebola katika eneo la Afrika Magharibi.

Pamoja na kutoa mchango mkubwa wa kuwahudumia waathirika kwa ugonjwa huo lakini watumishi hao wanaandamwa na matukio ya kukatishwa tamaa kama vile vitendo vya kunyanyapaliwa.

Akisisitizia juu ya haja ya kuwajali watumishi hao wa afya, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Margaret Chan amesema kuwa hakuna sababu kwa mtumishi wa afya kupoteza maisha wakati akiokoa maisha ya wengine. Alitaka

jamii kuwajali watumishi hao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud