Wakuu wa IAEA na OCHA watembelea Iran

18 Agosti 2014

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA Yukia Amano ametembelea Iran jumapili, tarehe 17, kwa ajili ya kutathmini mpango wa nyuklia nchini humo.

Amano amekutana na viongozi mbali mbali akiwemo rais wa Iran Hassan Rouhani, na amejadili naye jinsi ya kuongeza ushirikiano wao wakati Iran inatekeleza makubaliano ya November mwaka jana, ambapo imekubali kudhibiti matumizi ya nyukia na kutotumia nyuklia kwa masuala ya kijeshi.

Kwa mujibu wa bwana Amano, Iran imejitahidi sana na imeshachukua hatua zingine, Mwezi Mei mwaka huu, ili kuimarisha uwazi kwenye uhusiano huo.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Bi. Valerie Amos, naye ametembelea Iran siku hiyo hiyo ili kuzungumzia jinsi Iran inaweza kukabiliana na mizozo ya kibinadamu, kama mfano ile ya Iraq au Syria iliyosababisha watu milioni kadhaa kutafuta hifadhi katika nchi jirani za Mashariki ya Kati.

Bi Amos amesema, anaamini kwamba nchi ya Iran inaweza kuchangia kikubwa katika kuyasaidia mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwafikia watu wa Syria wanaohitaji msaada wa kibinadamu.