Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Mfanyakazi wa kibinadamu auawa na watoto wake watekwa nyara na LRA

UN Photo/Devra Berkowitz
Moustapha Soumare,

DRC: Mfanyakazi wa kibinadamu auawa na watoto wake watekwa nyara na LRA

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. DRC Moustapha Soumare, amelaani vikali mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wanamgambo wa Lords Resistance Army, LRA, tarehe 12 mwezi huu, maeneo ya Mayangu, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Soumare ambaye pia ni Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, amekaririwa akisema kuwa katika mashambulizi hayo mfanyakazi mmoja wa shirika la kimataifa Medair aliuawa na watoto wake watatu walitekwa nyara.

Taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA huko DRC imesema kuna ripoti kwamba watu wengine wameuawa au kutekwa nyara ikiwa ni tabia ya LRA katika mashambulizu yake, lakini bado idadi haijathibitishwa.

Soumare amepeleka rambirambi zake kwa familia za wahanga na akiwaomba wanamgambo wa LRA kuachilia huru waliotekwa.

Halikadhalika amesema LRA ndiyo chanzo cha ukosefu wa usalama katika mkoa huo unaopakana na Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mwaka 2013 zaidi ya watu 30 waliuawa na 180 wametekwa nyara.

Soumare ameongeza kwamba kitendo hicho kinapaswa kukumbusha jamii ya kimataifa juu ya hatari zinazokabili wafanyakazi wa huduma za kibinadamu.