UNMISS yalaani mapigano huko Bentiu

15 Agosti 2014

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS imesema kuwa alfajiri ya leo kumekuwepo na mapigano makali yaliyofanyika kwa kutumia silaha ndogo na vifaru eneo la kusini mashariki mwa makao ya ujumbe huo mjini Bentiu jimbo la Unity.

Kaimu Mkuu wa UNMISS Toby Lanzer amesema wakati wa mapigano hayo, zaidi ya raia 340 walikimbia makazi yao na kutafuta usalama kwa wanajeshi wa UNMISS walioko kwenye uwanja wa ndege.

Wanawajeshi wa UNMISS waliweza kuwapa ulinzi na baadaye kuwasindikiza hadi kambi ya UNMISS ya kuhifadhi wakimbizi iliyoko nje Bentiu.

Bwana Lanzer ameonyesha sikitiko lake na kulaani mapigano hayo na akasema kuwa UNMISS imechukua hatua za haraka kulinda raia na sasa inawapokea kwenye kituo chake.

Ametaka wanaohusika na mashambulizi ya leo kujiepusha na ghasia zaidi pamoja na vitendo vingine vinavyoweza kukwamisha UNMISS kulinda raia na mashirika ya kibinadamu kusambaza misaada.