Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waasi wa FDLR wakataa kambi ya mpito ya Kisangani

Ray Virgilio Torres, mkuu wa ofisi ya MONUSCO kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini, akihesabu silaha zilizorudisha na kundi la FDLR. PIcha ya MONUSCO.

Waasi wa FDLR wakataa kambi ya mpito ya Kisangani

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, umeelezea kusikitishwa sana na maamuzi ya FDLR kukataa kwenda kwenye kambi ya Kisangani.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ilikuwa imechagua eneo hilo la Kisangani kwa ajili ya operesheni za kujisalimisha waasi hao.

Akizungumza na Radio OKAPI, Mkuu wa ofisi ya MONUSCO katika mkoa wa Kivu Kaskazini Ray Virgilio Torres, amesema maamuzi hayo ni dalili ya kuonyesha kwamba FDLR wanataka kuendelea kupigana:

“ Sisi tunasikitika sana kwa sababu inatia mashaka juu ya utashi wa FDLR wa kujisalimisha. Nataka kuwakumbusha kwamba wao ndio walikuwa wameamua kujisalimisha, walisema tutaacha kupigana na tutaanza kupigana kwa njia nyingine bila kutumia silaha au ghasia”

Torres amesema kwamba Martin Kobler, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, aliweka wazi kwamba FDLR wasipojisalimisha MONUSCO itaweza kutumia nguvu za kijeshi dhidi yao.

Tayari askari 200 wa FDLR na watu 400 wanaowategemea kuishi, wapo kwenye kambi za MONUSCO, wakisubiri kurudishwa Rwanda .