Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani yakamilisha uteketezaji wa kemikali zihusianazo na Sarin kutoka Syria

Meli ya kimarekani, Cape Ray ambako kemikali zimeteketezwa. (Picha-OPCW)

Marekani yakamilisha uteketezaji wa kemikali zihusianazo na Sarin kutoka Syria

Shirika la kimataifa la kutokomeza silaha za kemikali, OPCW limesema tani zote za ujazo 581 za kemikali za sumu ambazo zingaliweza kutumiwa na Syria kutengeneza gesi ya Sarini zimetekezwa.

Mkurugenzi Mkuu wa OPCW Ahmet Üzümcü amesema shehena hiyo iliyosafirishwa kutoka Syria mwezi Julai iliteketezwa ndani ya meli ya kimarekani Cape Ray iliyokuwa kwenye eneo la kimataifa la bahari ya Mediteraniani.

Ameshukuru Marekani kwa mchango wake wa kutokomeza mpango wa silaha za kemikali wa Syria ikiwemo hatua hiyo ya kuteketeza kemikali hiyo kwenye mazingira salama.

Kwa sasa meli hiyo imeanza mchakato wa kuharibu tani za ujazo 19.8 za kemikali aina ya Sulfur, shehena ambayo ndiyo iliyobakia pekee kwenye meli hiyo na mchakato huo ukikamilika shehena hiyo itakwenda kutupwa kwenye eneo la ardhi huko Finland na Ujerumani.