Wataalam wa afya wakutana kutathmini maadili ya matibabu ya Ebola

11 Agosti 2014

Jopo la wataalam wa maadili ya utabibu wamekutana mjini Geneva kutathmini mchango wa matibabu ya majaribio katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Akiwahutubia waandishi wa habari mjini New York, Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema kuwa kuwatibu hivi karibuni wahudumu wawili wa afya kwa kutumia dawa za majaribio, kumeibua mjadala kuhusu ikiwa dawa ambazo hazijajaribiwa na kuthibitishwa kuwa salama kwa matibabu ya binadamu zinapaswa kutumiwa katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola.

“Jopo hilo lilijadili ikiwa ni jambo la uadilifu kutumia dawa ambazo hazijasajiliwa na ambazo madhara yake hayajulikani kwa matibabu ya watu, na ni vigezo gani vinapaswa kutumiwa kufanya uamuzi wa matumizi hayo. Chini ya uongozi wa Shirika la Afya Duniani, hatua zinazochukuliwa sasa katika nchi zote nne zilizoathiriwa ni kuzuia na kudhibiti maambukizi, uchagizaji wa jamii na kuwasaka watu ambao wamegusana na wagonjwa wa Ebola.”

Tangu ulipolipuka magharibi mwa Afrika, ugonjwa wa Ebola umewaua takriban watu 1000 katika nchi za Guinea, Liberia, Sierra Leone na hivi karibuni, Nigeria.