Ban akaribisha hatua za kuunda serikali Iraq

11 Agosti 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha hatua zilizopigwa katika kuunda serikali mpya nchini Iraq. Ban amempongeza pia Rais Fuad Massoum kwa kumkabidhi Dkt. Haider al-Abbadi mamlaka ya kuunda serikali mpya, kulingana na katiba ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu pia amemsihi Waziri Mkuu huyo kuunda serikali jumuishi ambayo itakubalika na jamii zote za Iraq, na ambayo inaambatana na utaratibu wa kikatiba.

Aidha, Bwana Ban ameelezea kusikitishwa na kuongezeka hali tete kisiasa, ambayo pamoja na tishio la sasa kutoka kwa kundi la kiislamu la msimamo mkali, ISIL, vinaweza kulitumbukiza taifa hilo katika matatizo makubwa zaidi.

Amesema watu wa Iraq wanastahili kuishi katika taifa salama, linalonawiwi na tulivu, akitoa wito kwa makundi ya kisiasa na wafuasi wao kuwa watulivu na kuheshimu harakati za kisiasa zinazodhibitiwa na katiba.