Sitisho la mapigano Gaza ni fursa ya kushughulikia sintofahamu ya pande zote:Ban

11 Agosti 2014

Tangazo la Misri kwamba Israeli na Palestina zimekubaliana sitisho la mapigano kwa siku tatu kuanzia usiku wa Jumapili kwa saa za Mashariki ya Kati, limekaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Sitisho hilo lisilo na masharti yoyote ni kwa misingi ya kibinadamu ambapo Bwana Ban amekaririwa na msemaji wake akisema kuwa anaamini kwa dhati kuwa hatua hiyo ni fursa nyingine kwa pande mbili hizo, chini ya uratibu wa Misri kukubaliana sitisho la kudumu la mapigano kwa maslahi ya jamii za pande zote.

Amesema huo pia ni mwanzo wa kushughulikia mizizi ya machungu ya pande zote mbili na ametka wahusika wote kushirikiana kwa dhati kumaliza hali ya sasa na kuepuka hatua zozote zinazoweza kusababisha kurejea tena kwa ghasia.

Katibu Mkuu amerejelea utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia kutekeleza makubaliano yatakayoimarisha amani na kuruhusu ujenzi na maendeleo kwenye Ukanda wa Gaza, mambo ambayo amesema yanahitajika sana.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter