Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Undeni serikali itakayoweza kukabiliana na ISIL: Ban awaeleza viongozi wa Iraq

UN Photo.
Katibu Mkuu Ban Ki-moon. Picha@

Undeni serikali itakayoweza kukabiliana na ISIL: Ban awaeleza viongozi wa Iraq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema bado ana hofu kubwa juu ya hali ya kibinadamu na kiusalama inavyoendelea kuibuka huko Iraq kila uchao wakati huu mchakato wa kupata waziri mkuu ukiendelea.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Ban akisema kuwa Umoja huo na jamii ya kimataifa inafuatilia kwa karibu hali ya kisiasa nchini humo na kutoa wito kwa vyama vyote vya kisiasa kuzingatia ratiba ya kikatiba iliyowekwa ya kumchagua Waziri Mkuu.

Katibu Mkuu ametaka busara itumike katika uchaguzi huo huku akiwasihi viongozi wote nchini Iraq kuunda serikali yenye wigo mpana inayokubalika na vikundi vyote nchini humo.

Amesema serikali ya aina hiyo inapaswa kuwa na uwezo wa kuhamasisha taifa kukabiliana na kitisho cha kikundi cha waislamu wenye msimamo mkali wanaotaka kujitenga na kuunda eneo lao, ISIL  kwa njia ambayo italeta usalama na utulivu nchini kote.