Baraza la Usalama lalaani ukiukwaji wa makubaliano ya amani Sudan Kusini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea kusikitishwa na kuzorota zaidi kwa hali ya kisiasa na usalama nchini Sudan Kusini, pamoja na janga la kibinadamu linalotokana na mzozo wa kisiasa ndani ya serikali ya SPLM, na machafuko, yakiwemo ukatili dhidi ya raia tangu tarehe 15 Disemba 2013.
Katika taarifa iliyotolewa na rais wake, Baraza la Usalama limelaani ukiukwaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha uhasama yaliyosainiwa mnamo Januari 23, 2014, na kusisitiza kuwa vitendo vya Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani ambaye sasa ni mpinzani, Riek Machar, vya kuandama suluhu la kijeshi kwa mzozo huo havikubaliki.
Baraza hilo limetoa wito wa dharura kwa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani, Riek Machar na pande zote kutekeleza makubaliano ya kuutatua mzozo wa Sudan Kusini yaliyotiwa saini mnamo Mei 9, 2014, na kushiriki kikamilifu katika mazungumzo ya amani yanayoendelea mjini Addis Ababa Ethiopia, na kutimiza ahadi zao za kuweka serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ifikapo tarehe iliyowekwa ya ukomo ya Agosti 10, 2014.
Pia Baraza hilo limelaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea pamoja na ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, vikiwemo vile vya mauaji kinyume na sheria, ukatili wa kulenga makabila, ukatili wa kingono, ubakaji, usajili wa watoto katika jeshi, uenezaji wa hofu miongoni mwa raia na mashambulizi dhidi ya shule, hospitali na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa.