Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waonya kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu nchini Iraq

@Ravina Shamdasani/OCHR

UM waonya kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu nchini Iraq

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa vitendo vya watu kulazimishwa kuhama makazi yao huko Kaskazini mwa Iraq vyaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu.

Imesema makumi ya maelfu ya raia kutoka jamii ya Yezidi na jamii nyingine ndogo wamekuwa wakisaka hifadhi kwenye milima ya Sinjar mpakani wa Iraq na Syia wakikwepa ghasia wanazofanyiwa na wanamgambo wa kiislamu wenye msimamo mkali, ISIL.

Mashirika ya misaada yamesema hali ya kibinadamu miongoni mwa wakimbizi wa ndani inazidi kudorora kwani familia zimenasa milimani bila chakula, maji na hata hazina mawasiliano na maeneo mengine.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu mjini Geneva.

“Kuenea kwa mashambulizi yenye mpangilio dhidi ya raia kwa misingi ya makabila, dini au imani ni uhalifu dhidi ya binadamu. Pande zote ikiwemo ISIL, vikundi shirika vilivyojihami vinapasaw kuzingatia sheria za kibinadamu za kimataifa, ikiwemo wajibu wao wa kulinda raia. Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa na serikali ya Iraq na ile ya eneo la Kurdi kuchukua hatua zote zinazowezekana kuhakikisha ulinzi wa raia, hususan wale wanaotoka jamii za pembezoni.”

Wakati huo huo shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM limesema zaidi ya raia Milioni Moja wa Iraq wamepoteza makazi yao tangu mwanzo wa mwaka huu ambapo nusu yao ni katika kipindi cha miezi miwili iliyopita pekee.