Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine mateso yataendelea hadi ghasia zitakapositishwa: UM

UN Photo/Loey Felipe/NICA
Baraza la Usalama Picha@

Ukraine mateso yataendelea hadi ghasia zitakapositishwa: UM

Baraza la Usalama limekutana Jumanne kuhusu Ukraine, likielezwa na John Ging, Mkurugenzi wa operesheni za Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, juu ya hali ya kibinadamu nchini humo.

Ging amesema watu watazidi kuteseka iwapo ghasia hazitasitishwa nchini humo, na hatua zinahitajika kuchukuliwa ili kuzuia mzozo unaoendelea kuzorotesha hali ya usalama.

Amesema Watu milioni 3.9 wanaishi kwenye maeneo yaliyoathirika na ghasia, mapigano yakiwa yameshaharibu miundombinu na upatikanaji wa maji na umeme.

Ametaja ripoti za Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa na ya Shirika la Afya Duniani WHO zinazoonyesha kwamba tayari watu wapatao 1,367 wameshafariki dunia, wakiwa ni askari au raia wa kawaida, na zaidi ya 4,000 wamejeruhiwa tangu mwanzo wa mzozo huo ulioibuka mwezi Aprili.