Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yalaani mauaji ya wahudumu zaidi wa kibinadamu Maban

UNMISS

UNMISS yalaani mauaji ya wahudumu zaidi wa kibinadamu Maban

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, umelaani vikali mauaji ya wafanyakazi watano wa mashirika ya kibinadamu yasiyo ya kiserikali nchini humo, ambayo yalitekelezwa na kundi linalojiita Kikosi cha Ulinzi cha Maban. Mauaji hayo yalifanyika mapema leo asubuhi karibu na mji wa Bunj, kata ya Maban, jimbo la Upper Nile.

Wawili kati ya wahanga hao waliuawa katika mji wa Bunj, na mwingine ametangazwa kutoweka, lakini anadhaniwa kufariki. Watatu wengine walifariki katika shambulizi la kuvizia wakirejea mjini Bunj.

Kundi la wanamgambo wa Maban limeripotiwa kuwalenga raia wenye asili ya Nuer, baada ya kupoteza wenzao katika kitali cha mapambano na wanajeshi wa Nuer.

Wahudumu wengi wa kibinadamu wamekimbilia maskani ya ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, huku machafuko hayo yakiwalazimu maelfu ya raia kuhama makwao, na wengi wao kutafuta usalama katika kambi ya wakimbizi ya Doro, iliyoko karibu na uwanja wa ndege.

UNMISS imetoa wito kwa mamlaka za mikoa, jimbo na kitaifa kuwafikisha mbele ya sheria watu waliotekeleza mauaji hayo haraka iwezekanavyo, na kudhibiti hali kwenye kata ya Maban.