Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Bunge jipya Libya ni ishara ya amani: UNSMIL

Picha@UNSMIL

Mkutano wa Bunge jipya Libya ni ishara ya amani: UNSMIL

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL umepongeza kitendo cha kufanyika kwa mkutano wa wawakilishi wapya wa Bunge nchini humo licha ya wakati huu mgumu na hali dhoofu ya usalama ikisema kuwa ni njia ya kuendeleza mazungumzo ya kisiasa licha ya chagamoto zilizopo.

Taarifa ya UNSMIL imesema hatua hiyo inadhihirisha kuwa raia wa nchi hiyo wanataka kuwe na utawala wa kidemokrasia, wa kisheria na heshima kwa haki za kibinadamu.

Hata hivyo imelaani umwagaji damu na mapigano yanayoendela jijini Tripoli na Benghazi ambayo yameathiri raia vibaya mno na kuchafua mazingira.

UNSMIL imezikumbusha pande zote husika kwenye mzozo huo kuwa zina jukumu la kulinda raia kulingana na sheria za kibinadamu za kimataifa na inasihi zisitishe mapigano na kutafuta suluhu ya tofauti zao kwa njia ya amani na siyo kwa mapigano.

Taarifa imesema kuwa ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa uko na imani na matarajio mema kuwa Bunge lililochaguliwa litajitahidi kutafuta amani ya kudumu kwa kuleta maridhiano baina ya pande zote zinazohusika.

Halikadhalika ujumbe umesema utaendelea kusaidia bunge hilo jipya kwa mbinu na mipango muhimu kulingana na mahitaji yao.