Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za afya zakaribia kuporomoka Gaza

Mtoto aliyejeruhiwa, hospitalini, Gaza. Picha ya @UNICEF

Huduma za afya zakaribia kuporomoka Gaza

 Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika maeneo yaliyokaliwa ya Palestina, James Rawley, ameonya kwamba hali ya afya inazorota kwa haraka sana kwenye ukanda wa Gaza.Pamoja na Mkurugenzi wa operesheni kwa ukanda wa Gaza wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Wa Palestina, UNRWA, Robert Turner, na Daktari Ambrogio Manenti, ambaye ni Naibu Mkuu wa ofisi ya Shirika la Afya Duniani WHO kwa Gaza, ameeleza kutiwa wasiwasi na ukosefu wa usalama kwa wauguzi na ndani za hospitali, akiongeza kwamba huduma za afya za dharura zinazidi kupatikana kwa shida kwa raia milioni 1.8 wa Gaza.

Amesema, theluthi moja ya hospitali imeshaharibika kwa sababu ya mapigano, na asilimia 40 ya wauguzi wanashindwa kufika kazini.

Juu ya hayo, hospitali zinazoendela kufanya kazi zimejaa, watu 8,000 wakiwa wameshajeruhiwa, na vifaa na madawa vimeanza kupungua.

Rawley amesisitiza sheria ya kimataifa ambayo inaweka wazi umuhimu wa kuheshimu shughuli za hospitali na wauguzi.