Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha uamuzi wa Afghanistan kutosajili watoto katika Jeshi

Nembo ya UNAMA

UM wakaribisha uamuzi wa Afghanistan kutosajili watoto katika Jeshi

Umoja wa Mataifa leo umekaribisha uamuzi wa serikali ya Afghanistan kuondoa na kuzuia uandikishaji au utumikishaji wa  watoto katika majeshi ya  nchi hiyo.

Serikali ya Afghanistan ilitoa hakikisho lake hivi karibuni la kuunga mkono mpango maalum wenye vigezo 15 vya kutekeleza mkakati uliotiwa saini na serikali hiyo na Umoja wa Mataifa, mwaka 2011. Mpango huo uliungwa mkono na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMA na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa UNAMA, Ján Kubiš ameipongeza serikali ya nchi hiyo kwa kukubali mpango huo maalum wa kuchukua hatua mathubuti ya kutoshirikisha watoto kwa majeshi na ulinzi wa nchi.

Jeshi la polisi ya Afghanistan limekuwa likiorodheshwa katika ripoti za Katibu Mkuu kuwa miongoni mwa vikosi vinavyosajili na kutumikisha watoto tangu mwaka 2010.

Serikali ya Afghanistan imeweka mkakati wa uchunguzi ili kuhakikisha kwamba watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wametolewa katika jeshi au polisi na hivyo kudhibiti hali hiyo kwa njia bora, amesema Bwana Kubis.

Mnamo Machi mwaka huu, Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na mizozo ya silaha, Leila Zerrougui, akishirikana na UNICEF walianzisha kampeni  ya kimataifa “Watoto, Siyo Wanajeshi” kama njia ya kukabiliana na kutokomeza tabia za serikali na wapiganaji kuandikisha na kushirikisha watoto katika vita ifikiapo mwaka 2016.