Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la mapigano kwa siku tatu Gaza matatani

Kituo cha usambazaji wa umeme , Gaza baada ya mashambulizi ya anga na Israeli katika kambi ya wakimbizi ya Nusseirat, Ukanda wa Gaza.Picha ya UM/Shareef Sarhan

Sitisho la mapigano kwa siku tatu Gaza matatani

Huko Mashariki ya Kati, pande zote husika kwenye mzozo huko ukanda wa Gaza zilikubali kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu, lakini jeshi la Israel limedai kwamba kikundi cha Hamas hakijaheshimu makubaliano hayo. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon pamoja na waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry walitangaza Alhamisi usiku kwamba pande zote zilikubali kusimamisha mapigano kwa kipindi cha saa 72 kuanzia Ijumaa asubuhi, kwa misingi ya kibinadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari hapa New York, msemaji wa Umoja ma Mataifa Stephane Dujarric amesisitiza umuhimu wa sitisho hilo akisema:

Sitisho la mapigano ni muhimu sana ili kuwapa raia muda wa kujizuia na ghasia. Wakati huo, raia huko Gaza watapata misaada ya dharura ya kibinadamu na fursa ya kutekeleza shughuli za msingi ikiwemo kuzika maiti, kutibu majeruhi na kutafuta vyakula.”

Mapema leo ijumaa Robert Serry, ambaye ni Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mashariki ya Kati, amearifu kwamba jeshi la Israel limeripoti kuwa askari wake wawili wameuawa katika kitendo kinachoonekana kuwa kinyume na makubaliano hayo.

Wakati huo huo mashirika ya kibinadamu yametoa wito kwa kufadhili msaada wa kibinadamu Gaza. dola milioni 369 zinahitajika ili kuwapatia mahitaji ya dharura raia milioni 1.8 wa Gaza.