Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama yaanza leo, UNICEF yatoa tamko

Picha: WHO/SEARO/Anuradha Sarup(UN News Centre)

Wiki ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama yaanza leo, UNICEF yatoa tamko

Leo Agosti Mosi ni mwanzo wa wiki ya unyonyeshaji watoto duniani ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hiyo ni mojawapo ya njia bora zaidi na rahisi ya kukuza watoto wenye afya na familia thabiti.

Maudhui ya mwaka huu yanaoanisha unyonyeshaji na mafanikio ya malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa.

Katika salamu zake Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amesema mtoto anaponyonya maziwa ya mama saa moja tu baada ya kuzaliwa kunaweza kuzuia kifo cha mtoto mmoja kati ya watano, pamoja na kuepusha utapiamlo wa utotoni.

Halikadhalika amesema mtoto kunyonya maziwa ya mama baada ya kuzaliwa husaidia makuzi ya ubongo wa mtoto pamoja na kuepusha utipatipwa wa baadaye na hata kudumaa.

Hata hivyo UNICEF inasema ni watoto wachache sana wanaopata fursa hiyo ya kunyonya maziwa ya mama zao baada ya kuzaliwa na ni wachache zaidi wanaopata fursa ya kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo wa uhai bila kupatiwa chakula kingine.

Kwa mantiki hiyo Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNICEF ametaka hamasisho zaidi kupitia siyo tu kwa jamii bali pia ngazi za kimataifa ili wakina mama wengi zaidi waweze kunyonyesha watoto wao kwani faida ni nyingi.