Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi Afghanistan, UNAMA yasifu uwepo wa wataalamu

Wapiga kura wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi, Afghanistan.Picha@UNAMA

Ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi Afghanistan, UNAMA yasifu uwepo wa wataalamu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA umekaribisha hatua ya kuwasili leo kwa waangalizi na wataalamu wa kimataifa nchini humo kabla ya kuanza hapo kesho kwa kazi ya ukaguzi wa matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais wa tarehe 14 Juni.

Mkuu wa UNAMA ambaye ni mwakilishi maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Afghanistan, Jan Kubiš amesema uwepo wao unadhihirisha nia ya dhati ya wadau wa kimataifa ya kutekeleza azma ya wagombea urais waliotaka mkwamo uliojitokeza umalizike kwa mamlaka husika kusaidiwa kukagua matokeo hayo.

Wakaguzi hao zaidi ya 200 watasimamia na kuishauri bodi ya tume huru ya uchaguzi Afghanistan juu ya mbinu bora zinazofaa wakati wa kuthibitisha, kuengua au kuhesabu upya kura husika zilizomo kwenye makasha 23,000 ya kupigia kura.

Miongoni mwao ni Jeff Fischer, mtaalamu mwandamizi wa kimataifa kuhusu chaguzi ambaye uzoefu wake na Umoja wa Mataifa ni pamoja na kuwa afisa mkuu wa uchaguzi wakati wa mashauriano ya umma huko Timor Mashariki.

Kwa mujibu wa makubaliano ya tarehe 12 Julai baina ya wagombea wawili wa Urais Dkt. Abdullah Abdullah na Dkt. Ashraf Ghani Ahmadzai ukaguzi wa kura utafanywa na tume huru ya uchaguzi mbele ya waangalizi wa kimataifa na kitaifa, mawakala wa wagombea, washauri kutoka Umoja wa Mataifa na vyombo vya habari.