Akiwa Costa Rica, Ban atoa mhadhara kuhusu sheria, haki na maendeleo endelevu

Katibu Mkuu Ban Ki-moon wakati alipokutana na Rais Luis Guillermo Solís, Costa Rica.Picha ya UM/Mark Garten/NICA

Akiwa Costa Rica, Ban atoa mhadhara kuhusu sheria, haki na maendeleo endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani nchini Costa Rica, leo ametoa mhadhara kwenye Mahakama ya Kikanda ya Haki za Binadamu, akiangazia ushirikiano wa taifa la Costa Rica na Umoja wa Mataifa, pamoja na fursa na changamoto zilizopo katika karne ya 21.

Hotuba ya Katibu Mkuu imejikita kwa masuala ya sheria na haki za binadamu, usalimishaji silaha na amani, pamoja na maendeleo endelevu. Ban amesema masuala hayo ambayo yanahusiana ndizo nguzo za Umoja wa Mataifa, na kwamba huwezi kulipuuza hata moja, ila zote zinapaswa kuzingatiwa kwa kina.

Bwana Ban amesema nchi zote zinapaswa kuhakikisha kuwa watu wa asili wanawakilishwa katika maamuzi kuhusu jinsi ya kutumia rasilmali asili na kujenga miundo mbinu katika maeneo yao ya asili, pamoja na maamuzi kuhusu maendeleo, mabadiliko ya tabianchi na masuala mengine ya kipaumbele duniani.

Ban amelisifu taifa la Costa Rica kwa kuzingatia haki za binadamu na demokrasia, pamoja na kuendeleza haki za makundi yaliyo hatarini. Amelisifu pia kwa kuendeleza usawa wa jinsia, na kwa hatua linazozichukua kutambua usawa wa watu wote bila kujali jinsia yao au mienendo yao kimapenzi.