Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wa Roma ("Gypsies") wanapaswa kulindwa- wataalam wa UM

Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng

Watu wa Roma ("Gypsies") wanapaswa kulindwa- wataalam wa UM

Wakati wa kumbukizi ya miaka 70 ya mauaji ya kimbari ya watu wa Roma, wataalam wa Umoja wa Mataifa wameziomba nchi zote duniani ziwakumbuke watu hao.

Watu wengi hawajui kwamba watu wa Roma, ambao pia wanajulikana kwa jina la “Gypsies” walilengwa na serikali ya Nazi, iliyotawala Ujerumani na sehemu mbalimbali za Ulaya wakati va vita vikuu vya pili vya dunia.

Serikali ya Ugerumani wakati ule ilifunga na kuua maelfu ya waroma katika sehemu zilizokaliwa za Urusi na Serbia, na kwenye kambi zao.

Adama Dieng, ambaye ni Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari na Rita Izsak, ambaye ni mtaalam maalum kuhusu maswala ya walio wachache, wamezishauri serikali zote za nchi ambapo mauaji hayo yalitokea wakumbuke uhalifu huo wa kimbari kwa kuifanya tarehe 2, Agosti siku ya kumbukizi ya kitaifa.

Siku hiyo, mwaka 1944, serikali ya Ujerumani iliamua kuua kwa njia ya gesi waroma 2,897 waliobaki kwenye kambi ya Auschwitz.

Wataalam hao wawili wamesema bado Waroma wanakumbwa na unyanyapaa katika baadhi ya nchi za Ulaya, na ubaguzi dhidi ya wahamiaji wenye asili ya kiroma unazidi siku hizi. Wameziomba serikali zichukue hatua za kulinda haki za watu hao.