Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama wa chakula yaendelea kudorora Sudan Kusini

Lori likisafirisha mbegu za FAO. Picha:FAO/CAR

Hali ya usalama wa chakula yaendelea kudorora Sudan Kusini

Juhudi za kutoa misaada kwa wakulima, wavuvi na wafugaji nchini Sudan Kusini zinakumbwa na matatizo kwa sababu ya upungufu wa ufadhili huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa janga la njaa katika baadhi ya maeneo, limeonya Shirika la chakula duniani, FAO. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Kufikia sasa, FAO imepokea dola milioni 42 za kimarekani kati ya dola milioni 108 ilizoomba kwa mpango wa mahitaji ya dharura mwaka 2014. Ufadhili uliopokelewa umezisaidia takriban familia 205,000 zilizo hatarini na zaidi ya watu milioni 1.2 kwa kutoa pembejeo, vifaa vya uvuvi na dawa za tiba ya mifugo.

Mnamo mwezi Mei takriban watu milioni 3.5, yaani mtu mmoja kati ya watatu nchini Sudan Kusini, alikuwa katika hatari ya usalama wa chakula huku idadi hii ikitarajiwa kupanda kufikia milioni 3.9 kati ya mwezi Juni na Agosti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la watoto duniani, UNICEF Anthony Lake, amabaye alikuwa ziarani nchini Sudan Kusini amesema kwamba hili ni jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua.

Yale tuliyoyaona Malakal huenda yanafanyika katika sehemu nyingi Sudan Kusini. Nina matumaini kwamba hatutasubiri mpaka pale janga la njaa litakapotangazwa nchini humo ndipo watu wachukue hatua. Lakini nina hofu kwamba tusipojitahidi zaidi basi huenda Sudan Kusini ikatumbukia kwenye janga la njaa.”

FAO inahitaji dola milioni 66 ili kuweza kutoa misaada kwa raia wa Sudan Kusini wanaokumbwa na wakati mgumu.