Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu mradi wa nishati endelevu Nicaragua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa azuru mradi wa nishati mbadala.Picha ya UM/Mark Garten/NICA

Ban asifu mradi wa nishati endelevu Nicaragua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani Amerika ya Kusini, ameusifu mradi wa taifa la Nicaragua wa nishati mbadala itokanayo na nguvu za upepo, ambao ukimalizika utakuwa na uwezo wa kukidhi robo ya mahitaji yote ya nishati nchini humo. Mradi huo unalenga kupunguza uvushaji wa gesi chafuzi kwa tani laki moja kila mwaka.

Akielezea kufurahishwa na kujifunza mengi kutokana na alichokiona, Ban amesema mradi huo wa Nicaragua unaingiliana vyema na mkakati aliouzindua wa nishati endelevu kwa wote miaka mitatu iliyopita, na ambao unaungwa mkono na zaidi ya nchi 80 zinazoendelea. Mkakati huo unalenga kuwezesha watu kote duniani kupata umeme ifikapo mwaka 2030, kuongeza maradufu ubora wa uzalishaji wa nishati, ikiwemo nishati mbadala.

Nishati ya kisasa ndio ufunguo wa kubadili maisha ya watu. Inaweza kuboresha hali ya maisha na inaweza kutumiwa kuendeleza utu wa mwanadamu, na inaweza pia kuchangia kupunguza ukatili. kliniki na hospitali zinaweza kuwezeshwa zaidi kunusuru maisha. Mitaa ikiwa na mwangaza wa kutosha usiku, inaweza kupunguza ukatili wa kingono dhidi ya wanawake. Watoto wanaweza kusoma usiku.”

Baadaye leo Katibu Mkuu ameelekea Costa Rica, ambako atakutana na Rais Luis Guillermo Solís, Waziri wa Mambo ya Nje, Manuel González Sanz, na wawakilishi wa makundi ya watu wa asili, na baadaye kutoa mhadhara kwenye mahakama ya haki za bindamu.