Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani Nicaragua, Ban atoa wito kwa nchi zilinde haki za wahamiaji

Ban ahutubia wanahabari wiki karibuni. Picha ya UM

Ziarani Nicaragua, Ban atoa wito kwa nchi zilinde haki za wahamiaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa nchi zote zisaidie katika kulinda utu na haki za wahamiaji, hususan watoto, huku akiyalaani vikali makundi ya wahalifu wanaowasafirisha watoto hao kwa njia haramu yakiwaweka hatarini pamoja na kuwanyanyasa.

Bwana Ban ambaye yuko ziarani nchini Nicaragua, amesema kuwa taifa la Nicaragua limeonyesha uongozi mzuri katika kushirikiana na nchi jirani zake kukabiliana na hali ya kibinadamu ya dharura inayiwakabili makumi ya maelfu ya watoto wahamiaji kutoka Amerika ya Kati, hasa kutoka nchi za El Salvador, Guatemala na Honduras.

Akikutana na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Rais Daniel Ortega wa Nicaragua, Katibu Mkuu amelisifu taifa hilo katika kuendeleza uchumi wake na ujumuishaji wa kijamii, na kwa hatua lilizopiga katika kufikia malengo ya maendeleo ya millennia, zikiwemo kuwawezesha wanawake na mipango ya kuongeza nishati mbadala.