WHO yaomba dunia “kufikiria tena”ili kukabiliana na virusi vya homa ya ini

28 Julai 2014

Leo Julai 28  ni siku ya Homa ya Ini (Hepatitis) Duniani ambako Shirika la afya duniani WHO na wadau wanachagiza watunga sera, wahudumu wa afya na umma, “kufikiria tena” kuhusu ugonjwa huu unaouwa kimya kimya.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii WHO imekaribisha hatua mpya zilizopigwa katika kukabiliana na ugonjwa huo. Homa ya ini, au hepatitis, hupatikana katika aina tano tofauti, A, B, C, D na E, na huathiri mamilioni ya watu kote duniani, yakisababisha ugonjwa ini na kusababisha vifo vya watu milioni 1.4 kila mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Margaret Chan, amesema kuwa ugonjwa huo umepuuzwa kwa miaka mingi, lakini sasa kuna uelewa mkubwa na msukumo mpya wa kimataifa kukabiliana nao.

Msukumo huu mpya ulichagiza mjadala kuhusu hepatitis kwenye Baraza la Dunia la Afya 2014, ambako nchi 194 ziliunga mkono azimio la kuongeza juhudi za kuzuia, kupima na kutibu homa ya ini ya virusi vya hepatitis. Azimiohilolinasisitiza umuhimu wa nchi kubuni mikakati ya kina ya kukabiliana na hepatitis, pamoja na dawa mpya zinazoweza kutibu hepatis B na C, na pia kutoa wito kwa WHO kutafuta njia za kuutokomeza ugonjwa huo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud