Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laomba ufadhili haraka kuepusha baa la njaa Sudan Kusini

Mapigano yanayoendelea Sudan Kusini yameleta madhila makubwa ikiwemo njaa kwa wakazi hususan wanawake na watoto. (Picha-WFP)

Baraza la Usalama laomba ufadhili haraka kuepusha baa la njaa Sudan Kusini

Wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea kusikitishwa na tatizo kubwa la kutokuwepo usalama wa chakula Sudan Kusini, ambalo sasa ndilo baya zaidi kote duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na rais wa Barazahilo, Eugène-Richard Gasana, wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea hofu kubwa kuwa tatizohiloSudan Kusini huenda karibuni likafikia kiwango cha baa la njaa, kwa sababu ya kuendelea mapigano, kuwalenga raia na kuwalazimisha watu kuhama makwao.

Wametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo kwa pamoja ziliahidi ufadhili wa zaidi ya dola milioni 618 kwa Sudan Kusini na kwa ukanda mzima kwenye kongamano la ahadi za ufadhili, Oslo Norway, kutimiza ahadi zao haraka, na kuongeza ufadhili wao. Wamesema kuwa fedha hizo zinahitajika kwa dharura sasa, ili kutoa usaidizi wa kunusuru maisha katika hali hiyo mbaya ya kibinadamu nchini Sudan Kusini.

Wanachama wa Baraza la Usalama pia wametoa wito kwa pande zinazozozana kuheshimu na kuwalinda raia, kujiepusha na vitendo vya machafuko yanayowalenga raia, husasan wanawake na watoto, na kuruhusu haraka ufikishaji misaada ya kibinadamu kwa walengwa, kulingana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.