Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Sudan Kusini hawawezi kusibiri njaa itangazwe ndipo dunia ichukue hatua: UNICEF na WFP

Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Ertharin Cousin. Picha: WFP(UN News Centre)

Watoto Sudan Kusini hawawezi kusibiri njaa itangazwe ndipo dunia ichukue hatua: UNICEF na WFP

Wakuu wa Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa wameonya leo kuwa watoto Sudan Kusini hawawezi kusubiri hadi baa la njaa litangazwe nchini humo, ndipo jamii ya kimataifa ichukue hatua.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF na yule wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Ertharin Cousin, wamesema kuwa walikutana na watoto wenye utapiamlo uliokithiri walipowazuru akina mama na watoto walioathiriwa na mzozo katika mji ulioharibiwa na mapigano wa Malakal, ambapo makumi ya maelfu ya watu bado wanaishi katika maskani ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa..

Wakuu hao wamesema wana hofu kuwa jamii ya kimataifa inaruhusu marudio ya kile kilichofanyika Somalia na Pembeni mwa Afrika miaka mitatu iliyopita, wakati onyo za mapema za njaa iliyokithiri na utapiamlo kuongezewa zilipuuzwa, hadi pale viwango rasmi vya njaa vilipotangazwa.

Takriban watoto milioni moja chini ya umri wa miaka mitano watahitaji kutibiwa kwa utamiamlo uliokithiri mwaka huu wa 2014 nchini Sudan Kusini, kwa mujibu wa UNICEF na WFP. UNICEF imeonya kuwa jamii ya kimataifa isipotoa msaada unaohitajika sasa ili kuongeza juhudi za utoaji misaada ya chakula na lishe, takriban watoto 50,000 huenda wakafa kutokana na utapiamlo mwaka huu.