Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Iraq alaani uharibufu wa Urithi wa kihistoria mjini Mosul

wakimbizi wanaoendelea kukimbia mapigano Mosul @UNHCR Inje Colijn

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Iraq alaani uharibufu wa Urithi wa kihistoria mjini Mosul

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Nickolay Mladenov, leo amelaani vikali vitendo vya kuharibu urithi wa kihistoria, likiwemo kaburi la Nabii Yona na Msikiti wa Mosul pamoja na majengo mengine muhimu ambayo yameorodheshwa na kuhifadhiwa kama urithi unaoonyesha utamaduni wa nchi hiyo.

Amesema kuwa utesaji wa kupangwa wa walio wachache nchini humo, na uharibifu wa urithi wa utamaduni, pamoja na kuteketeza kabisa sehemu muhimu za kihistoria na zile takatifu kwa kidini za Kikristo na Kiislamu, kunaonyesha kuwa ISIL haijali kabisa ubinadamu. Amesema vitendo kama hivyo ni lazima vilaaniwe na jamii ya Kimataifa na viongozi wa kisiasa, kidini na umma nchini Iraq kwa ujumla.

Bwana Mladenov amesema kuwa matukio ya hivi karibuni ni thibitisho kuwa, lengo la makundi ya kigaidi ni kuharibu urithi na sura ya nchi hiyo.

Halikadhalika, Mladenov amsema kwamba vitendo vya kundi la ISIL vya kuteketeza makanisa, misikiti na vitu vya umuhimu mkubwa katika mji wa Mosul, vinafaa kutoa msukumo kwa wanasiasa na viongozi wote nchini humo kutafuta suluhu la haraka ili kurejesha na kulinda hadhi ya nchi hiyo.