Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji haramu wa binadamu unahatarisha maisha ya wahamiaji- IOM

Picha:UNHCR/A. Rodriguez

Usafirishaji haramu wa binadamu unahatarisha maisha ya wahamiaji- IOM

Wahamiaji wa asili ya kiafrika  na waomba hifadhi wananyanyapaliwa mikononi mwa wasafirishaji haramu katika safari ya kuvuka bahari ya mediterenia wakielekea Ulaya, limesema Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM.

Wahamijai hao kutoka Afrika waliookolewa na wanajeshi wanamaji wa Italia, mnamo Jumamosi iliyopita, wamesema kwamba walikumbana na ubaguzi wa rangi, kudungwa visu na walikuwa wamerundikana kwenye boti bila makoti ya kuokoa maisha.  

Ripoti zinasema kwamba boti hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya watu 750 lakini ni watu 569 tu ndio waliokolewa.

Aidha, kuna ripoti kwamba kulikuwa na vurugu ndani ya boti ambako wahamiaji kadhaa walirushwa ndani ya maji.

IOM inasema kwamba wahamiaji kutoka Afrika walikuwa wakilipa dola za kimarekani 900 kwa ajili ya kusafirishwa hadi Ulaya, huku waSyria  wakilipa bei hiyo maradufu.

Flavio Di Giacomo ni msemaji wa IOM, Roma.

"Walikuwa wamefika kutoka Ngeria, Niger, Mali, Ivory Coast na Gambia, wengi ni vijana, wako kati ya umri wa miaka 18-24. Ni vijana wanaosaka maisha bora Libya na baadaya Ulaya.Wengi wanasema wanakimbia machafuko nyumbani. Kuna watu walioondoka Mali mwaka mmoja uliopita na hawakujua kwamba marafiki zao walikuwa wamepotea kwa hivyo tuliwaambia huenda labda wamefariki, basi walisikitika sana."

IOM inahimiza jamii ya kimataifa kutoa mpango mbadala kwa wale wanaohatarisha maishayaobaharini ikiwemo utaratibu unaofuata sheria  kwa wahamiaji wanaosaka hifadhi.