Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya amani CAR yasainiwa Brazzaville

Picha@WFP/George Forminyen

Makubaliano ya amani CAR yasainiwa Brazzaville

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika ya Kati, Abdoulaye Bathily, na yule kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Babacar Gaye, wamekaribisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande zote za mzozo unaoendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yalisainiwa jana tarehe 23 Julai, katika mkutano ulioandaliwa Brazzaville, Congo.

Wawakilishi hao wawili wa Umoja wa Mataifa wameridhishwa na hali iliyopo Brazzaville, wakisema hatua inayofuata ni kuandaa mazungumzo kwa ngazi ya kitaifa, na kongamano la kitaifa la maridhiano na ujenzi mpya wa nchi.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu Ban Ki Moon amemteua Diane Corner kuwa Naibu Mwakilishi wake maalum kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Naibu mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA.

Diane Croner ni raia wa Uingereza ambaye sasa hivi ni balozi wa Uingereza nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Baraza la Usalama limekaribisha kusainiwa kwa makubaliano hayo ya kusitisha uhasama na machafuko, na kutoa wito kwa pande zote husika kuyatekeleza makubaliano hayo mara moja.