Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana nchini Iraq hatarini kukeketwa kwa nguvu

Picha@UNHCR/S.Baldwin

Wanawake na wasichana nchini Iraq hatarini kukeketwa kwa nguvu

Zaidi ya wanawake milioni 4 kazkazini mwa Iraq wanakabiliwa na hatari ya kuketwa, kwa mujibu wa viongozi wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Kundi la Waislamu wenye msimamo mkali, ISIS, ambalo linatawala eneo hilo la Iraq limeripotiwa kutoa amri wanawake wote wafanyiwe ukeketaji.

Mratibu wa Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Jacqueline Badcock, amesema amri hiyo ni ya kwanza ya aina hiyo kwa sababu ukeketaji wa wanawake si kitu cha kawaida Iraq.

Ukeketaji wa wanawake si tabia iliyoenea Iraq. Baadhi ya visa vimeripotiwa maeneo ya Kurdistan. Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu UNFPA limekadiria kwamba wanawake na wasichana milioni 4 wanaweza kuathiriwa na fatwa hiyo mpya. Hiyo si hiari ya raia wa Iraq wala ya wanawake wanaoishi kwenye mazingira hayo magumu yaliyokaliwa na magaidi”

Mwaka 2012, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalokataza ukeketaji kwa kusema ni ukiukwaji wa haki za wanawake na wasichana.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu milioni 1.2 wamekimbia makwao kaskazini na katikati mwa Iraq tangu mwanzo wa mapigano.