Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa UM alaani mauaji ya mbunge mwingine Somalia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, Nicholas Kay

Mwakilishi wa UM alaani mauaji ya mbunge mwingine Somalia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Somalia, Nicholas Kay, amelaani mauaji ya Saado Ali Warsame, mbunge wa kike katika Bunge la Somalia, na kuelezea kusikitishwa mno na mashambulizi yanayoendelea kuwalenga wabunge katika mji wa Mogadishu.

Bi Warsame na dreva wake walifyatuliwa risasi na kuuawa wakisafiri kwenye gari leo Mogadishu. Pamoja na kuwa mbunge, Bi Warsame alikuwa mwimbaji maarufu ambaye kifo chake kitawagusa wengi kote nchini Somalia.

Akilaani mauaji hayo, Bwana Kay amesema mchango wa wanawake wa Somalia katika jamii ni lazima ulindwe na kuheshimiwa na wote. Ametoa wito kwa mamlaka za Somalia kufanya kila liwezekanalo kuwawajibisha waliotenda uhalifu huo kisheria.