Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wataka baa la wakimbizi wa ndani Nigeria lishughulikiwe

Chakola Bayani (Picha@UN/NICA)

Wataalam wa UM wataka baa la wakimbizi wa ndani Nigeria lishughulikiwe

Watalamu wawili wa haki za kibinadamu wametoa wito kwa serikali ya Nigeria na jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya hatma ya wakimbizi zaidi ya Milioni 3.3 wa ndani nchini humo kwa sababu ya machafuko tangu mwaka 2010. Idadi hiyo ni mojawapo ya idadi ya juu zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani.

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kibinadamu za wakimbizi wa ndani, Chakola Bayani, amesema ulinzi wa na usaidizi wa kimataifa kwa wakimbizi hao umekuwa haba, na haujalingana na kasi ya kuongezeka kwa wakimbizi wa ndani nchini Nigeria. Amesema kulazimika kuhama kwa idadi kubwa ya watu limeendelea kuwa tatizo sugu nchini humo.

Beyani amesisitiza kuwa kuzuia watu kuhama zaidi, uteketezaji wa makazi ya raia kiholela na kurushwa kwa makombora katika maeneo ya biashara na ya halaiki ya watu ni lazima kupewe kipaumbele.

Naye Rita Izsak, Mtaalam Maalum kuhusu haki za walio wachache ameeleza kuwa wengi wa watu waliolazimika kuhama ni watu wa makabila au dini za walio wachache, ambao wamekuwa waathiriwa wa ukatili.

Watalamu hao wamehimiza pande zote husika katika mgogoro kuheshimu raia na makazi yao, kwani wengi wao ni wanawake na watoto ambao wamepitia machungu mengi, na wengi wa wanawake hao ni wajane wanaowalea watoto peke yao.

Watalamu hao wameihimiza serikali ya Nigeria kuweka sera mwafaka inayoangazia wakimbizi wa ndani ili itumike kama njia mojawapo ya kusuluhisha tatizo hilo nchini humo, na wakiongeza kuwa hili ni jambo la umuhimu mkubwa. Wameitaka pia serikali ya Nigeria kutafuta suluhisho la kudumu kwa raia wake waliotimuliwa kutoka makwao.

Halikadhalika, wameipongeza serikiali hiyo kwa juhudi za hivi karibuni za kuwasaidia wakimbizi zaidi ya 200,000.