Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Picha za wanawake na watoto wanaouawa na kuteseka Gaza zinavunja moyo: Ban

Zaidi ya wakimbizi 50,00 wantafuta hifadhi katika shule za UNRWA.Picha ya Shareef Sarhan/UNRWA/maktaba

Picha za wanawake na watoto wanaouawa na kuteseka Gaza zinavunja moyo: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani Mashariki ya Kati, amesema picha za wanawake na watoto wanaouawa na kuteseka Gaza zinatia uchungu moyoni, akiongeza kwamba ni vigumu kustahmili kuziona.

Ban amesema hayo akikutana na waandishi wa habari akiambatana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina. Awali, Bwana Ban alikuwa Israel, ambako alikutana na Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, na kisha kulihutubia Baraza la Usalama, ambako alishuhudia Mwakilishi wa Palestina akionyesha picha za watoto waliouawa kwa wanachama wa Baraza hilo.

Katibu Mkuu amesema kuwa raia wengi mno wanauawa katika mapigano, na familia nyingi hazina njia ya kukwepa madhila ya mzozo huo.

Amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wapalestina, UNRWA, linawapa hifadhi zaidi ya watu 100,000, ambao ni takriban asilimia 5 ya idadi nzima ya watu Gaza.

Amesema operesheni za kijeshi za Israel Gaza ni lazima zikomeshwe, na mashambulizi ya roketi kutoka Gaza pia ni lazima yakomeshwe. Amesema juhudi zaidi zinatakiwa kuwalinda raia, na mapigano hayo kusitishwa mara moja.