Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM linaendesha mkutano pamoja na Sekritariati ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu ili kusanifisha utaratibu wa kutunza na kusaidia waathirika wa biashara hiyo haramu.
Tanzania ni moja ya nchi zilizokumbwa na shida ya usafirishaji haramu wa watoto, wakiwa ni wasichana wanaotumikishwa manyumbani kama watumwa, wanawake wanaolazimika kufanya biashara ya ngono, au vijana wanaotumikishwa mashambani.
Shughuli ya kwanza ya IOM Tanzania ni kupambana na biashara hiyo haramu, kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania, polisi, waendesha mashtaka wa serikali, ofisa wa mambo ya kijamii na wadau mbalimbali. Shirika hilo limefanikiwa kurejesha kwao msichana mmoja aliyetumikishwa kufanya biashara ya ngono China.
Ingawa usafirishaji haramu wa binadamu bado ni tatizo kubwa kwa Tanzania, nchi hiyo imefanikiwa kuchukua hatua mbalimbali katika kupambana na uhalifu huo, tangu kupitishwa kwa sheria maalum, 2008.