Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laomba mapigano yasitishwe Gaza

UN Photo/Paulo Filgueiras
Mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati.

Baraza la Usalama laomba mapigano yasitishwe Gaza

Baraza la Usalama leo limekutana kujadili kuhusu mzozo unaoendelea baina ya Israel na Palestina, Katibu Mkuu Ban Ki Moon akilihutubia Baraza hilo kutoka Ramallah, Palestina, baada ya kutembelea nchi ya Israel. Katibu Mkuu amekaribisha jitihada za viongozi wote wanaojituma katika utaratibu wa kufikisha makubaliano ya kusitisha mapigano.

Aidha, amelaani mashambulizi yaliyofanyika na jeshi la Israel kwenye maeneo ya Shejaiyah, huko Gaza akilaani vilevile mashambulizi yanayotekelezwa na kundi la Hamas dhidi ya raia wa Israel. Amerejelea ujumbe wake kwa pande zote za mzozo:

“ Kwanza sitisheni mapigano. Pili, anzeni kuongea, na Tatu, shughulikieni mizizi ya tatizo lenu. Ni lazima kusitisha mapigano, lakini bila kushughulikia matatizo ya awali, hatutatatua shida hiyo, tutaiahirisha mpaka ghasia nyingine”.

Mwakilishi maalum wa nchi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, naye amelihutubia baraza la usalama kwa kulikumbusha kuhusu hali ya kibinadamu huko Gaza, akilaani vikali vitendo vya Israel dhidi ya Gaza.

Ameanza kutokwa na machozi akionyesha picha za wahanga na watoto waliouawa katika mashambulizi hayo, akiorodhesha majina ya watoto hawa 121, huku akisema:

“ Sisi si nambari, ni binadamu. Wakati damu ya wahanga ikimwagika hospitalini, wakati tunasikia kelele za maumivu ya majeruhi, tunajua kwamba jamii ya kimataifa imeshindwa. Imeshindwa kutimiza jukumu lake la kulinda raia kwenye mizozo na imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa Umma”

Ameliomba Baraza la Usalama lilaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina na kuwapatia raia wa Palestina ulinzi wa kimataifa.

Kwa upande wake, mwakilishi wa kudumu wa Israel, Ron Prosor, amesema jamii ya kimataifa inapaswa kutambua ukweli ulio mbele yake, akisema:

“ Angalia dunia leo, na utaona kwamba hatari ya kwanza kwa amani ya dunia inaliangalia baraza hilo machoni. Kutoka Buenos Aires mpaka Brussels, Benghazi mpaka Boston, hakuna nchi ambayo inaepuka na hatari ya uislamu wenye msimamo mkali. Waasi hawa, wakiwa na itikadi kali na silaha za kuua, wanaendeleza vita ili kuharibu maisha na matumaini ya watu”.

Amesema nchi yake ndiyo ya pekee katika ukanda wa Mashariki ya Kati kuwa na serikali ya uhuru na demokrasia, ambayo inapambana na vikundi vya kiislamu vyenye msimamo mkali.  Ameishutumu Hamas kwa kuhatarisha maisha ya Waisrael ikiwa imesharusha zaidi ya roketi 10,000 kwenye nchi yake kwa kipindi cha miaka 10 na kujenga njia za chini ya ardhi ili kufika katikati ya vijiji vya Israel.

Juu ya hiyo, amesema, Hamas hailindi maisha ya Wapalestina, lakini mbali na hayo, inarusha roketi kutoka shule, miskiti na hospitali, kuliko kulinda usalama wa raia wake. Israel, Prosor ameeleza, ilikuwa haitaki kushambulia Palestina na raia wake. Na hivi mkutano wa baraza la usalama unaendelea.