Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu mpya za UNICEF zaonyesha haja ya kuchukua hatua dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni

Akiwa na mwaka mmoja, Fatima alikeketwa akiwa kijijini kwake katika mkoa wa Afar, Ethiopia ambayo ina idadi kubwa zaidi ya ukeketaji. Picha: UNICEF/Kate Holt.(UN News Centre)

Takwimu mpya za UNICEF zaonyesha haja ya kuchukua hatua dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni

Kongamano la kwanza kabisa la watoto wa kike linafanyika leo mjini London, Uingereza, kuzivalia njuga mila mbili potofu zinazoathiri mamilioni ya watoto wa kike kote duniani: ukeketaji wa wanawake na ndoa za utotoni. Taarifa kamili na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Dhamira ya kongamano hilo ni kuchagiza uongezaji kasi kwa hatua za kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni. Kongamano hilo limeandaliwa na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, likishirikiana na serikali ya Uingereza.

Takwimu zilizotolewa leo na UNICEF  zinaonyesha kuwa, huku kuenea kwa desturi hizo kukiwa kumepungua kidogo katika miongo mitatu iliyopita, kasi ya hatua za kuzitokomeza inapaswa kuongezwa kwa kiasi kikubwa, ili kulingana na viwango vya ongezeko la idadi ya watu katika nchi ambako bado tabia hiyo imetanda.

Zaidi ya wasichana na wanawake  milioni 130 wamekabiliwa na aina moja au nyingine ya ukeketaji katika nchi 29 Afrika na Mashariki ya Kati, ambako mila hiyo imeshamiri. Zaidi ya wanawake milioni 700 walio hai sasa, waliolewa wakiwa watoto, milioni 250 katiyaochini ya umri wa miaka 15.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake, amesema kuwa ukeketaji na ndoa za utotoni hudhuru watoto wa kike daima, kwa kuwanyima haki ya kufanya maamuzi yao wenyewe na kufikia viwango vya juu zaidi vya uwezo wao. Ameongeza kuwa vitendo hivyo vinadhuru sio tu wasichana hao, bali pia familia na jamii zao.

Ameongeza kuwa watoto wa kike hawapaswi kuchukuliwa kama mali, na wana haki ya kujiamulia hatma yao.