Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatiwa hofu na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya Gaza

Mtoto huyu wa kipalestina asimama nje ya nyumba iliokuwa nyumba yao iliyoharibiwa baada ya mashambulizi ya angani kambini mji wa Rafhakusini mwa Ukanda wa Gaza (Julai 12)© UNICEF/NYHQ2014-0911/El Baba

WHO yatiwa hofu na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya Gaza

Vituo vya afya vipatavyo 18 vimeharibiwa Gaza, huku wahudumu 20 wa afya wakijeruhiwa wakati mashambulizi ya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas yakiendelea. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa limesikitishwa mno na kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, likitoa wito kwa pande zote katika mzozo kutimiza wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ambayo inapinga mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, magari na wahudumu wa afya, pamoja na wagonjwa.

WHO imesema wahudumu wa afya ni lazima walindwe wakati wote, na kuruhusiwa kufanya kazi zao. Fadella Chaib kutoka WHO amesema kuwa idadi kubwa ya majeruhi imezidi uwezo wa vituo vya afya ambavyo awali vilikuwa vikitoa huduma kwa hali ya kawaida.

“Kuna hofu kubwa kuhusu vifaa vya matibabu, kwani kuna uhaba wa dawa na vifaa vinginevyo katika hospitali za wizara ya afya na za mashirika yasiyo ya kiserikali kwa sababu ya idadi kubwa ya wahanga na uhaba uliokuwepo hata kabla ya machafuko kuchacha. Kule Gaza, WHO inafuatilia mahitaji katika hospitali, yakiwemo ya dawa na vifaa vinginevyo kila siku, na inashirikiana na wadau wa afya na wafadhili kuongeza vifaa hivyo.

Kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya Wapalestina 3,500, wakiwemo watoto 1,100 na wanawake 608 wamejeruhiwa.