Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila kisa cha utumikishwaji wa watoto vitani ni janga kwa jamii: MONUSCO

Martin Kobler@UN

Kila kisa cha utumikishwaji wa watoto vitani ni janga kwa jamii: MONUSCO

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikitolewa leo kuhusu hali ya watoto walioathirika na mzozo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Mkuu wa Ujumbe wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, Martin Kobler, amesema kwamba mbali na takwimu, kila kisa cha uhalifu huo ni janga kwa mtoto, kwa familia na kwa jamii nzima. Amesema amewahi kujadili na watoto waliopigana pamoja na waasi, wakiwa na silaha za kuwashinda urefu, wakihadithia jinsi waliovyolazimishwa kutekeleza mauaji.

Ameongeza kwamba, ingawa mafanikio yameanza kuonekana katika kulinda watoto na utumikishwaji huo, bado kesi nyingi zinapaswa kusikilizwa. Ameiomba serikali ya DRC kufuatilia na kupeleka mbele ya sheria watekelezaji wa uhalifu huo, wakitoka kwa jeshi la serikali ama vikundi vya waasi.

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya watoto walioathirika na mzozo, DRC, imeonyesha kwamba takriban watoto 4200 walitumikishwa na waasi nchini humo.