Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujerumani yapiga jeki UNICEF kuendeleza haki za watoto Libya

Watoto wakiingia shule iliyomo ndani ya tenti la UNICEF katika kambi la Shousha mpakani mwa Libya na Tunisia. UNICEF/Heifel Ben Youssef.(UN News Centre)

Ujerumani yapiga jeki UNICEF kuendeleza haki za watoto Libya

Serikali ya Ujerumani imetoa kiasi cha euro 100,000 kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Watoto, UNICEF, ili kuliwezesha shirika hilo kutekeleza miradi yake nchini Libya.

Kiasi hicho cha fedha kitasaidia kufanikisha kampeni ya kitaifa inayotekelezwa sasa nchini Libya ya lengo la kuwezesha watoto kutambua haki zao. Makabidhiano ya fedha hizo yamefanyika mjini Tripoli baina ya Balozi wa Ujerumani nchini Libya, Christian Much na mwakilishi wa UNICEF nchini humo Ghassan Khalil.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, mwakilishi huyo wa UNICEF alipongeza kutolewa kwa msaada huo akisema kwamba umetolewa wakati muafaka haswa wakati ambako taifa linapitia katika kipindi kigumu. Pamoja na mambo mengine, fedha hizo zinatazamiwa kuendeleza taasisi za kisheria na utoaji maamuzi ili kuziwezesha kutekeleza mifumo inayotoa ulinzi kwa watoto.