Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu kujadilia hali ya Gaza

Baraza la haki za binadamu kujadilia hali ya Gaza

Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linatazamia kukutana jumatano wiki hii kwa ajili ya kujadiili hali ya mambo katika ukanda wa Gaza.

Kikao hicho kimeitishwa kwa pamoja kati ya Misri na Pakistan na kuungwa mkono na nchi wanachama 15 za baraza hilo. Miongoni mwa nchi hizo zilizounga mkono ni pamoja na China, Cuba, Urusi na Afrika Kusini.

Hapo siku ya Jumapili Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa wito likitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwa hivi sasa anazuru eneo hilo kuonyesha utayari wa Umoja wa Mataifa kuzisaidia pande zinazopigana kufikia makubaliano ya kuleta amani.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi wa Palestina UNRWA limesema kuwa hadi kufikia sasa kiasi cha Wapalestina 81,000 wameomba hifadhi ya kikimbizi katika makazi yanayofikia 61.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa mapigano hayo yamesabisha zaidi ya Wapalestina 500 wameuawa tangu Israel ilipoanza mashambulizi yake ya kijeshi katika ukanda wa Gaza.