Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani kutunguliwa kwa ndege ya Malaysia

UN Photo/Loey Felipe
Baraza la Usalama wakichukuwa dakika ya ukimya kwa walio athirika na ndege MH17.

Baraza la Usalama lalaani kutunguliwa kwa ndege ya Malaysia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja, limepitisha azimio la kulaani vikali tukio la kutunguliwa kwa ndege ya Malaysia, MH17, mnamo Julai 17 kwenye jimbo la Donetsk Oblast, nchini Ukraine, ambalo lilisababisha vifo vya watu 298.

Baraza la Usalama limepeleka tena risala za rambi rambi kwa familia za wahanga wa tukio hilo, na watu na serikali za nchi zao za asili.

Katika azimio hilo pia, Baraza la Usalama limeeleza kuunga mkono juhudi za kuanzisha uchunguzi huru na wa kina kuhusu tukio hilo, kulingana na mwongozo wa kimataifa wa usafiri wa angani. Katika muktadha huo, Baraza la Usalama limeelezea kusikitishwa na ripoti za wataalam kutoruhusiwa ipasavyo kufika kwenye eneo la tukio.

Azimio la leo pia limeyataka makundi yenye silaha yanayodhibiti eneo la mkasa huo na maeneo ya karibu kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kutatiza uchunguzi, vikiwemo kuondoa bidhaa za wahanga na vifaa vingine muhimu.

Baraza la Usalama pia limetaka shughuli zote za kijeshi zikomeshwe mara moja, ili kuruhusu uchunguzi salama wa wachunguzi wa kimataifa.