Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika 10 yatuzwa kwa juhudi za kupambana na Ukimwi

Picha@UNAIDS

Mashirika 10 yatuzwa kwa juhudi za kupambana na Ukimwi

Mashirika kumi ya kijamii yameshinda tuzo ya Red Ribbon ya mwaka 2014, kutokana na juhudi za kutoa msukumo katika kupunguza athari za maradhi ya Ukimwi.

Tuzo hiyo imetolewa kwenye kikao maalum cha kongamano la kimataifa la 20 kuhusu Ukimwi mjini Melbourne, Australia. Mashirika yaliyoshinda tuzo hiyo mwaka huu yametoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC, Guyana, Indonesia, Iran, Kenya, Lebanon, Malawi, Nepal, Ukraine na Venezuela.

Tuzo ya Red Ribbon ndiyo tuzo ya juu zaidi inayotolewa kwa juhudi bunifu za kijamii za kukabiliana na maradhi ya Ukimwi. Mashirika ya kijamii yameonyesha ulimwengu jinsi ya kuchagiza jamii kubadilika katika kukabiliana na Ukimwi, na juhudi hiyo inatambua ufanisi wa mashirika hayo.