Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka machafuko mapya Sudan Kusini yakomeshwe

Ban ataka machafuko mapya Sudan Kusini yakomeshwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ameelezea kusikitishwa sana na shambulizi lililofanywa leo na vikosi vya waasi wa SPLA Upinzani vilivyo chini ya Makamu wazamani wa rais, Riek Machar kwenye mji wa Nassir, jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.

Shambulizi hilo ni la kwanza tangu serikali na Bwana Machar waliporejelea makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo Juni 10, 2014. Katika taarifa iliyo tolewa na msemaji wake, Bwana Ban amesema shambulizi hilo linadhoofisha juhudi zinazoendelea za kikanda na kimataifa za kuelekea kuanza tena mazungumzo ya kisiasa na suluhu la amani kwa mzozo wa Sudan Kusini.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa Bwana Machar kusitisha mara moja operesheni zote za mashambulizi kwenye mji wa Nassir na maeneo mengine, na kwa serikali ya Sudan kujiepusha na kufanya mashambulizi ya kujibu vitendo vya waasi wa Machar. Amezikumbusha pande zote kuhusu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Ban amewaonya pia viongozi waasi wa SPLA Upinzani kuwa watawajibika ikiwa raia wowote wasio na hatia au walinda amani wa Umoja wa Mataifa watapata madhara yoyote yanayosababishwa na vikosi vyao.

Katibu Mkuu amezitaka pande zote kukomesha machafuko mara moja, na kuanza mazungumzo ya kisiasa na kuonyesha utashi wa kisiasa kupata suluhu la amani kwa mzozo uliopo.