Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani, Ban akutana na viongozi wa Mashariki ya Kati Rais Abbas

Ban na Rais Abbas wakiwa Doha, Qatar: Picha ya UM/Eskinder Debebe

Ziarani, Ban akutana na viongozi wa Mashariki ya Kati Rais Abbas

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa ukanda wa Mashariki ya Kati, akiwemo Rais Mahmoud Abbas wa Palestina na Amiri wa Qatar.

Baadaye, akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Khalid Bin Mohamed Al-Attiyah, amekutana na waandishi wa habari na kuelezea kusikitishwa kwake na nyakati za mtihani mkubwa na hali tete wanayokabiliana nayo watu wa Mashariki ya Kati.

Ban amesema raia wengi sana wanafariki huku wanawake wengi na watoto wakiwa wahanga wa mashambulizi maovu mno.

Ban amesema watu wengi wanaishi kwa uoga wa mashambulizi, na kulaani shambulizi la Israel la hii leo ambalo limewaua raia wengi, wakiwemo watoto katika mtaa wa Shejaiyah, Gaza.

Ban ameitaka Israel kujizuia, na kujitahidi zaidi kuwalinda raia, huku akizitaka pande zote kwenye mzozo huo kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu

Ban amesema machafuko hayo ni lazima yakomeshwe mara moja, huku akitaja mchango muhimu ambao Qatar inaweza kutoa katika juhudi za kuutatua mzozo huo.