Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani utesaji wa makundi ya walio wachache Mosul, Iraq

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon. @UN-Maktaba

Ban alaani utesaji wa makundi ya walio wachache Mosul, Iraq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amelaani vikali utesaji wa kupangwa wa makundi ya walio wachache nchini Iraq, unaotekelezwa na wafuasi wa waasi wa Jamhuri ya Kiislamu Iraq (IS) na makundi husika yaliyojihami. Bwana Ban amesikitishwa hasa na ripoti za vitisho kwa Wakristo Mosul na maeneo mengine yanayodhibitiwa na ISIL nchini Iraq, vikiwemo vya kuwataka ama wajisilimishe, walipe ushuru, waondoke au wauawe hivi karibuni.

Ripoti nyingine zinazotia ghadhabu ni kwamba watu wa jamii za Turkoman, Yazidi na Shabak wanakabiliwa na hatari ya kutekwa, kuuawa na kuharibiwa kwa mali zao, huku nyumba za Wakristo, Washia na Shabak zikiwa zimetiwa alama.

Ban amesema kuwa katika wiki chache zilizopita, makundi ya walio wachache ambayo yameishi katika mikoa ya Mosul na Ninewa kwa miaka mingi, yamekuwa yakishambuliwa na ISIL na makundi husika yaliyojihami.

Katibu Mkuu amerejelea ujumbe wake kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya raia au makundi ya kiraia kwa misingi ya kabila, dini au dhehebu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, na wale wanautenda ni lazima wakabiliwe na mkono wa sheria. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na serikali ya Iraq na ile ya jimbo la Kurdistan kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya waliolazimika kuhama makwao.