Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msemaji wa WHO afariki kwenye ajali ya ndege ya Malaysia

Glenn Thomas, Picha ya WHO

Msemaji wa WHO afariki kwenye ajali ya ndege ya Malaysia

Watu 298 wamefariki dunia kwenye ajali ya ndege ya Malaysia iliyotokea tarehe 17, Julai, akiwemo Glenn Thomas, mfanyakazi wa Shirika la Afya Duniani, WHO.

Glenn Thomas ambaye alikuwa msemaji wa WHO alipanda ndege hiyo kwa ajili ya kuhudhuria kongamano la kimataifa kuhusu ukimwi litakaloanza wiki ijayo, nchini Australia.

Gregory Hartl, msemaji wa WHO, amesema Glenn Thomas alikuwa mwandishi wa habari ambaye alifanya kazi na BBC kabla ya kuungana na WHO, ambapo alikuwa anawasiliana na wawakilishi wa mitandao mbalimbali na kuelimisha watu kuhusu shughuli za WHO

“ Dada yake amesema amefariki akifanya kazi anayoipenda. Thomas amefanya kazi na WHO kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10. Tutamkumbuka kwa ucheshi wake na upendo wake kwa maswala ya afya. Wale ambao wamekuwa na fursa ya kumjua na kufanya kazi naye watamkumbuka sana. Ameacha mume wake Claudio na dada pacha wake Tracey”.

Wafanyakazi wengine wa UNAIDS na watalaam wa ukimwi wengine wanadaiwa kuwa wamefariki pia katika ajali hiyo. Tayari kifo cha Joep Lange kimethibitishwa, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi, UNAIDS. Joep Lange alikuwa mwalimu maarufu na mtafiti wa zamani kuhusu maswala ya ukimwi.