Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC haifuatilii viongozi wa Afrika tu, bali wa dunia nzima: Msemaji wa ICC

Fadi El-Abdallah, Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC. Picha@UNIFEED

ICC haifuatilii viongozi wa Afrika tu, bali wa dunia nzima: Msemaji wa ICC

Wakati Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC imeaadhimisha hapo jana miaka 16 tangu kusainiwa kwa mkataba wa Roma ulioiunda mahakama hiyo, msemaji wake, Fadi El-Abdallah, ameiambia Redio ya Umoja wa Mataifa kwamba ICC imeshaaminika na nchi nyingi duniani, kwani tangu kuwepo kwa ICC mwaka 2002, idadi ya nchi wanachama imeongezeka kutoka 60 hadi 122.

“Tumeona kwamba nchini wanachama wanaamini kazi za ICC kwa sababu zimeanza kututumia ushahidi kuhusu kesi zao, na kuiomba ICC isaidie kuwapa wahanga haki zao, hii ikionyesha uaminifu kwa kazi za ICC na haja ya sheria ili kujenga amani endelevu.“

Halikadhalika, amesema watu wengi hawaelewi kazi za ICC, wakifikiria kwamba ICC inafuatilia zaidi viongozi wa Afrika. Msemaji huyo ameeleza kwamba ICC haiwezi kufuatilia kesi kwenye nchi ambazo hazijaidhinisha mkataba wa Roma, kama mfano Syria, Marekani, Israel ama Urusi, akiongeza:

“ ICC inaendesha uchunguzi wa awali kuhusu kesi kumi zililizo kwenye mabara tofauti, Georgia, Ukraine, nyingine ikiwa kuhusu uhalifu unaodaiwa kufanywa na askari wa Uingereza nchini Iraq. Kwa hiyo ICC haizingatii Afrika pekee. Uchunguzi ulianza Afrika kwa sababu nchi za kiafrika zenyewe ziliiomba ICC kuanzisha uchunguzi huko”

Hatimaye, akizungumza kuhusu kesi iliyoanzishwa dhidi ya viongozi wa Kenya, amesema kesi ya Samuel Ruto imeshaanza wakati ile ya raisi Uhuru Kenyatta inatakiwa kuanza mwezi Oktoba.