Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya Mandela yazinduliwa rasmi, Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela

Tuzo ya Mandela yazinduliwa rasmi, Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limekutana mahsusi kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, kuenzi mchango wa Hayati Nelson Mandela kwa kukuza demokrasia, haki kwa watu wa rangi zote na maridhiano. Katika mkutano huo, tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Nelson Rolihlahla Mandela pia imezinduliwa rasmi.

Leo Julai 18 ni miaka 96 tangu kuzaliwa kwa Hayati Nelson Mandela, ambaye aliaga dunia Disemba mwaka jana. Tuzo ya Mandela, ambayo ilitangazwa baada ya kifo chake, inalenga kuwatambua watu wanaodhihirisha hulka ya Mandela, na ilianzishwa kwa pendekezo la Rais wa Baraza Kuu, John W. Ashe, ambaye leo amesema

Sauti ya Ashe

“Mwaka huu, kwa mara ya kwanza, tunaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake bila yeye. Lakini mioyo yetu inapobaki ba uzito wa kumpoteza, tumebaki na kumbukumbu isiyofutika ya sifa zake za kuendeleza. Mchango wake kwa ulimwengu ulikuwa mkubwa na wa maana mno, na jina lake litatajwa na watoto wetu, na wajukuu wetu.”

Naye Katibu Mkuu Ban Ki-Moon, amesema Siku ya Mandela ni siku ya wito wa kuchukua hatua.

“Kila mmoja wetu anaweza kusheherekea siku hii kwa kusaidia kukabiliana na matatizo halisi ya jamii zetu. Pamoja, tunaweza kufanya maadhimisho yetu kuwa na maana zaidi kwa kufungua njia za mustakhbali bora zaidi.”

Wengine waliozungumza kwenye mkutano wa leo ni Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Kasisi Jesse Jackson, maarufu kwa kupigania haki na kumaliza ubaguzi Marekani.

Kila tarehe 18 Julai, watu kote duniani huhimizwa kujitoa kwa dakika 67 kuwahudumia wengine hospitalini, kufundisha watoto, kutoa chakula kwa wasio na makazi na huduma nyingine kwa jamii. Katibu Mkuu, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wale wa Ubalozi wa Afrika Kusini kwenye UM, wameadhimisha siku hii kwa kuitunza miti iliyopandwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na katika jamii ya Harlem Mashariki, New York.